Rais Mstaafu wa awamu ya pili mzee Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa serikali inatambua matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee nchini na inafanya jitihada kubwa katika kuzitatua changamoto hizo.
Mzee Mwinyi ametoa kauli hiyo mkoani Arusha wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani humo, ambapo amemwakilisha Rais John Magufuli.
Kwa mujibu wa mzee Mwinyi, wazee nchini wana changamoto nyingi zinazotakiwa kushughulikiwa kwa haraka ikiwa ni pamoja na namna ya kupata huduma bora za afya na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyotokana na imani za kishikirina.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo ya siku ya wazee duniani, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, -Ummy Mwalimu amesema kuwa tayari serikali imeshaandaa sheria itakayosimamia maslahi ya wazee nchini.
Siku ya wazee duniani huadhimishwa Oktoba Mosi ya kila mwaka ambapo kauli mbiu kwa mwaka huu ni kuwaenzi watetezi wazee wa haki za binadamu kwa kuimarisha haki zao, kuzidisha utambuzi wao katika jamii na kutatua changamoto wanazopitia.