Siku ya Wauguzi Duniani yaadhimishwa leo

0
228

Tanzania leo inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Wauguzi, ikiwa nia hatua ya kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na wahuduma hao wa afya.

Kitaifa maadhimisho ya siku ya Wauguzi Dunaini yanafanyika mkoani Manyara na mgeni rasmi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu.

Katika ujumbe wake kwenye maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani, shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mchango wa Wauguzi ni mkubwa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi nyingi duniani zinakabiliwa na ugonjwa wa corona.

Limesema Wauguzi wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya corona pasipo kujali kuwa nao wapo hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa huo.

Licha ya jitihada za serikali kuendelea kuboresha sekta ya afya, wauguzi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni upungufu wa vifaa na vitendea kazi, idadi kubwa ya watu wanaohitaji huduma hospitalini, kupigwa, kutukanwa na kudhalilishwa na ndugu wa wagonjwa, na kupata magonjwa ya kuambukiza.

Siku ya Wauguzi Duniani, huadhimishwa Mei 12 ya kila mwaka, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taaluma ya uuguzi duniani Marehemu Florence Nightingale ambaye angekuwa anatimiza umri wa miaka 201 hii leo.