Siku ya pili ya ziara ya Rais wa Tanzania nchini Kenya

0
179
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride Ikulu ya Kenya, jijini Nairobi wakati wa ziara nchini humo.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo anaendelea na ziara yake nchini Kenya ambapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuhutubia mkutano wa jukwaa la wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania utakaojadili fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika nchi mbili hizo.

Halikadhalika, Rais anatarajiwa kulihutubia bunge la Kenya leo, katika siku yake ya pili na ya mwisho ya ziara nchini humo.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, Rais Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta wamekubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili na kufungua fursa mpya za kibiashara.

Miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni pamoja na mradi wa bomba la gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara, kuimarisha usafiri wa majini kupitia ziwa Victoria, reli na anga pamoja na kushughulikia vikwazo vya biashara.

Kampuni 513 za Kenya zimewekeza nchini Tanzania mtaji wa dola za Marekani bilioni 1.7 (sawa na shilingi za Tanzania trilioni 3.888) ambazo zimezalisha ajira 51,000 ilihali kampuni 30 za Tanzania zimewekeza nchini Kenya shilingi za Kenya bilioni 19.3 (sawa na shilingi za Tanzania Bilioni 410.233).