https://www.youtube.com/watch?v=wynBUZfsHeg&feature=youtu.be
Rais John Magufuli ameongeza muda wa siku Saba ili kuwawezesha Watuhumiwa wa Uhujumu Uchumi walio tayari kutubu na kurejesha fedha pamoja na mali zao, kufanya hivyo.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Ikulu Jijini Dar es salaam, wakati akipokea
taarifa ya utekelezaji wa ushauri alioutoa Septemba 22 mwaka huu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuangalia namna ya kuwasamehe Watuhumiwa wa Uhujumu Uchumi walio tayari kutubu na kurejesha fedha pamoja na mali zao.
Amesema kuwa, hatua ya kuongezwa kwa muda huo, itasaidia Watuhumiwa wengine ambao hawakufikia uamuzi wa kutubu, pamoja na wale ambao wamekwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vikwazo gerezani kufanya hivyo.
Rais Magufuli amesema kuwa, katika siku Saba alizotoa hapo awali, jumla ya Watuhumiwa 467 wameandika barua kwa DPP na kuomba kusamehewa ambapo fedha watakazolipa ni zaidi ya Shilingi Bilioni 107.
Ameshauri kuwa, Watuhumiwa hao wakimaliza taratibu za malipo hayo ni vema wakawa huru kuendelea na shughuli zao, kwa kuwa hiyo ndio maana ya msamaha.