Siku 150 za mbio za Mwenge wa Uhuru zaanza rasmi

0
150

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameuwasha Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Mwehe, Zanzibar Mei 17, ulipofanyika uzinduzi wa mbio hizo.

Akizungumza kuhusu kauli mbiu ya mbio hizi kwa mwaka huu ‘TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu Itumie kwa Usahihi na Uwajibikaji,’ Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezungumzia umuhimu wa TEHAMA nchini.

“Maendeleo na matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni muhimu katika sekta zote, kwani ni njia muhimu ya kuongeza ufanisi katika nyanja tofauti ikiwemo elimu, biashara pamoja na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kila siku zinazopelekea maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesisitiza Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla

Amemkabidhi mwenge huo Luteni Josephine Mwabashi, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2021.

Mwenge utazunguka mikoa 31, kwa siku 150 kuanzia leo, Mei 17 hadi Oktoba 14, 2021 ukianzia mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar na kuishia mkoani Geita, atakapokabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Jumla ya wakimbiza Mwenge kitaifa ni sita kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wakiwemo wanawake wawili.

Mwenge ni Ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanzania, ukimulika ndani na nje ya nchi, huku ukileta matumaini, heshima, amani na upendo kati yetu.