Shilingi bado tulivu dhidi ya dola

0
166

Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani imeendelea kuwa tulivu, ambapo dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,298.5 mwezi Aprili mwaka huu, ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,291.3 mwezi Aprili mwaka 2020.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2021/2022.

Amesema utulivu wa shilingi umetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa sera za fedha na bajeti, kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya nchi pamoja na mwenendo chanya wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Dkt. Nchemba ameongeza kuwa hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kusimamia misingi ya uwazi katika ununuzi na uuzaji wa fedha za kigeni nchini zimechangia thamani ya shilingi dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani kuwa tulivu.