Rais Samia Suluhu Hassan leo Juni 6, 2022 ameshuhudia utiaji saini wa miradi ya maji ya miji 28 Tanzania kati ya Tanzania na India.
India imeipatia Tanzania mkopo wa dola milioni 500 sawa na takribani shilingi trilioni 1.165 ambayo yote itaenda kwenye kutekeleza miradi ya maji kwa asilimia kubwa Tanzania Bara na kiasi kingine kikielekezwa Zanzibar.
Rais Samia amesema, “Mradi huu badala ya miji 16 tumekwenda mpaka 28. Kuna maeneo yalihitaji mabomba 6 tu, kwenye ‘design’ kuna mabomba 21. Vile mmerudi mmekaa vizuri mradi huu unakwenda kuwanuvaisha wengi.
“Hata miradi hii ambayo tunatekeleza sasa hivi, mmejitahidi sana kubana matumizi, pahali pa mradi mmoja, mradi mmoja unazaa fedha za kuanzia mradi mwingine. Asanteni sana na naomba endeleeni hivyo,”- ameongeza Rais Samia.
Naye Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema awali miradi hii ilielekezwa kufikia miji 16 Tanzania Bara na mji mmoja wa Zanzibar lakini kwa nguvu ya Rais Samia miradi itafikia miji 28.
Miji itakayonufaika ni pamoja na Wang’ing’ombe, Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani, Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Singida, Chemba, Chamwino, Kasulu, Chunya, Lujewa, Makambako, Kiomboi, Njombe, Manyoni, Mugumu Serengeti, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga, Newala, Tandahimba, Nanyamba, Rorya Tarime na Songea.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa leo amewasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ya zaidi ya shilingi bilioni 35.4
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma Waziri Mchengerwa amesema kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 8.2 ni Mishahara ,Bilioni 11.3 ni matumizi mengineyo na Bilioni 15.8 ni ya miradi ya Maendeleo.
Waziri Mchengerwa amesema kwa mwaka 2022/23 Wizara inatarajia kukusanya jumla ya Shilingi Milioni Mia Tisa (Sh.900,000,000) kupitia Idara ya Maendeleo ya Michezo ikiwa vyanzo vya mapato hayo ni pamoja na viingilio katika matukio ya michezo yanayofanyika katika viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, kukodisha kumbi na gym zilizopo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na ada za mafunzo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.
Aidha kwa upande wa Taasisi sita (6) zilizo chini ya Wizara hiyo kiasi kinachokadiriwa kukusanywa ni Shilingi Bilioni 5.3.
Waziri Mchengerwa ameongeza katika kuhakikisha Tanzania inakidhi vigezo vya kuandaa mashindano ya Kimataifa na Kikanda, Serikali katika mwaka 2022/23 imetenga kiasi cha Shilingi Billioni 10 kwa ajili ya Ukarabati wa viwanja na amesisitiza hatua ya kwanza vitaanza viwanja saba (7) vilivyopo katika Majiji, ambavyo ni Jamhuri – Dodoma, Sheikh Amri Abeid – Arusha, Sokoine – Mbeya, CCM Kirumba – Mwanza, na Mkwakwani – Tanga, ukarabati huo utavihusisha viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo ukarabati viwanja vingine ikiwa ni pamoja na kuweka nyasi bandia na majukwaa katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Mtwara, Iringa, Tabora na Shinyanga baada ya kujadiliana na wamiliki wa viwanja hivyo.
“Mkakati huu utaiwezesha kufanikisha Ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za Tanzania kuandaa mashindano makubwa ya mchezo wa soka ya Klabu Bingwa Afrika (AFCON) ambayo tayari Tanzania imependekezwa kuandaa kwa mwaka 2027”. amesema Waziri Mchengerwa