Shehena ya mafuta ya kula yakamatwa Pwani

0
1812

Jeshi la polisi mkoani Pwani limekamata lori moja lililokuwa linasafirisha shehena ya mafuta ya kula yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia bandari zisizo rasmi zilizopo katika wilaya ya Bagamoyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Pwani, – Wankyo Nyigesa amesema kuwa lori hilo aina ya Fuso lenye namba za usajili T 336 CVF limekamatwa katika kijiji cha Miono likiwa na watu wawili waliokuwa wakisafirisha mafuta hayo.

Kamanda Nyigesa amesema kuwa lori hilo limekamatwa baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema na baada ya polisi kulifuatilia waliweza kulikamata likiwa limebeba madumu 328 ya mafuta ya kula ambayo hayajalipiwa ushuru.

Ameongeza kuwa kukwamatwa kwa lori hilo ni sehemu ya msako unaofanywa na jeshi la polisi mkoani Pwani kwa lengo la kudhibiti bidhaa za magendo zinazoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru kupitia bandari 15 sizizo rasmi zilizopo katika wilaya ya Bagamoyo.

Amesema kuwa katika msoko huo, polisi pia wamekamata mifuko 50 ya sukari.