Shamba la Vikuge latakiwa kujiendesha kibiashara

0
129

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, ameagiza shamba la malisho ya mifugo lililopo Vikuge wilayani Kibaha mkoani Pwani kujiendesha kibiashara.

Naibu Waziri Ulega ametoa agizo hilo wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Pwani.

Pia ameliagiza shamba hilo la malisho ya mifugo lililopo Vikuge kusambaza mbegu za malisho kutoka nchini China ijulikanayo kama JUNCAO katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kuwa ina sifa ya kustahimili sehemu yenye ukame ili Wafugaji wapande malisho hayo.

Naibu Waziri Ulega amumuelekeza Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Profesa Elisante Ole Gabriel kuhakikisha aina mpya ya malisho hayo inasambazwa, na kusimamia vema ili mradi huo uweze kuwa na tija kwa Taifa hasa kwa wafugaji vijijini.

Amesema mbegu za malisho ya JUNCAO zisambazwe kuanzia ngazi ya mikoa, wilaya hadi vijiji lengo likiwa ni kudhibiti mifugo na Wafugaji kuhamahama kutafuta malisho.

Naibu Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesema hataki kuona mambo yanayoanzishwa kwa ajili ya kunufaisha Wananchi yanaishia njiani, kwani ni vizuri kukawa na mwendelezo wa teknolojia hiyo ya kilimo hicho kipya cha malisho ya mifugo hata kusambazwa kwa wafugaji hadi vijijini.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha mbegu za malisho hayo zinaenea hadi vijijini kwa Wafugaji akiwataja hasa wa mikoa yenye ukame kama Dodoma, Singida, Manyara, Shinyanga na iwapo zitasambazwa vizuri itapunguza tatizo la Wafugaji na mifugo yao kuhamahama kutafuta malisho ya mifugo yao.

“Kinachosababisha Wafugaji kuzunguka na kuhama hama ni kutafuta chakula cha malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao, hivyo kama Wafugaji watafikishiwa mahali walipo itawasaidia wafugaji kuwa na uhakika wa malisho.” amesema Naibu huyo wa Waziri Mifugo.