Shahidi wa 12 Kesi ya Mbowe atoa ushahidi kwa siku ya nne

0
144

Shahidi wa 12 katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Luteni Denis Urio ameendelea kutoa ushahidi wake katika mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa kuhojiwa na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala.

Shahidi huyo ambaye alianza kutoa ushahidi wake siku tatu zilizopita akiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Abdala Chavulla ameendelea kuweka wazi juu ya Mawasiliano yake na Mshitakiwa wa nne Freeman Mbowe ambaye alimpa jukumu la kuwatafuta vijana kwa ajili ya kazi maalum.

Katika ushahidi wake Luteni Denis Urio amedai kuwa alionana na Mbowe kwa mara ya kwanza mwaka 2012 jijni Dar es Salaam na baadaye alipohitaji vijana hao kwa ajili ya kazi alifanya hivyo huku akichukua tahadhari.

Shahidi huyo amedai katika mchakato huo alipokea jumla ya Shilingi 699,000 kutoka kwa Mbowe kwa ajili ya kuwawezesha vijana hao kununua nguo kisha kusafiri kwenda Moshi kwa ajili ya kazi maalum (VIP protection).

Aidha amedai mshitakiwa Freeman Mbowe alitaka kujua msimamo wake kwa vyama vya upinzani, lakini yeye akamjibu kuwa kutokana na taratibu wa kazi zake kama askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzanaia JWTZ, haruhusiwi kufungamana na chama chochote isipokuwa kwa kiongozi anayekuwa madarakani kwa wakati huo.

Ameongeza kuwa kutoka na maongezi hayo alishindwa kuvumilia hivyo kuamua kumweleza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Robert Boaz wakati huo hivyo kutakiwa kuendelea kumpa Mbowe ushirikiano huku akitoa taarifa hizo kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zingine za kiupelelezi.

Hata hivyo shahidi huyo ameomba mahakama iyapokee maelezo yake yawe sehemu ya ushahidi wake kwa upande wa Utetezi licha ya kuwepo kasoro chache kwenye vielelezo na maelezo ya shahidi huyo kutofautiana wakati akiendelea kuhojiwa.

Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili kuendelea kupokea ushahidi kwa shahidi huyo wa 12 kwa Upande wa jamhuri na washitakiwa wamerudishwa rumande.