Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – Standard Gauge awamu ya kwanza kutoka jijini Dar Es Salaam hadi Morogoro, umekamilika kwa asilimia 22 huku katika baadhi ya maeneo shughuli za ujenzi ukiwa umepiga hatua.
Licha ya kuwepo kwa changamoto katika mradi huo, shughuli za ujenzi wa mradi huo zinafanyika usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Katika kufuatilia maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa maarufu kama Standard Gauge, bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania –TRC wamefanya ukaguzi katika mradi huo kuanzia jijini Dar Es Salaam hadi Kilosa mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo kutoka jijini Dar Es Salaam hadi Morogoro inafanyika kwa saa 24 ili kuhakikisha mradi huo unajengwa na kukamilika kwa wakati.
TBC imeshuhudia baadhi ya madaraja yakiwa yamekamilia kwa zaidi ya asilimia 70 likiwemo daraja ambalo litawezesha njia ya reli kupita juu na sehemu ya chini ya daraja hilo itatumika kama barabara kwa ajili ya magari.