Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema kutekelezwa kwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza mkoani Kigoma hadi Kindu – Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kupitia Gitega – Burundi kutaongeza ufanisi katika matumizi ya ukanda huru wa biashara Barani Afrika.
Dkt. Mpango amesema hayo wakati akiongoza majadiliano na wawekezaji kuhusu mradi wa reli hiyo ya kisasa, majadiliano yaliofanyika katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika linaloendelea jijini Abidjan, Ivory Coast.
Amesema serikali zote tatu zimeweka nia ya dhati ya kutekeleza mradi huo ambapo kwa upande wa Tanzania tayari imekwishatekeleza miradi unganishi ya reli ya kisasa inayochagiza uwepo wa mradi huo muhimu.
Aidha Makamu wa Rais amesema asilimia 50 ya mizigo inayotoka katika bandari za Tanzania hupelekwa nchi za Burundi na DRC, hivyo uhitaji wa reli hiyo ya kisasa ni muhimu kwa sasa.
Amesema uwepo wa idadi watu inayokadiriwa kufikia milioni 170 katika mataifa ya Tanzania, DRC na Burundi ni uhakika wa soko kwa bidhaa mbalimbali zitakazosafirishwa kupitia reli hiyo.
Makamu wa Rais ameutaja mradi huo kama njia mojawapo ya kuhifadhi mazingira kutokana na kutumia nishati ya umeme pamoja na kuimarisha sekta ya kilimo na bidhaa zake katika ukanda uliojaaliwa ardhi yenye rutuba na rasilimali watu ya kutosha.
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Adesina Akinwumi amesema benki hiyo inaunga mkono kwa dhati utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa ambao utasaidia maisha ya watu barani Afrika.
Dkt. Adesina amesema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania , Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla katika ufanyaji biashara na kuinua uchumi baina ya mataifa katika ukanda huru wa biashara barani Afrika.