Serikali yawekeza Bilioni 3.5 Shule maalumu Patandi

0
236

Uwekezaji uliofanywa na serikali wa zaidi ya shilingi bilioni 3.6 wa ujenzi wa shule ya sekondari jumuishi Patandi umewanufaisha wanafunzi 168.

Shule hiyo ya bweni inajumuisha watoto wenye ulemavu wa viungo, uono hafifu, upofu, viziwi, ualbino, ulemavu wa akili na usonji imeanza kutoa elimu mwaka huu 2021 kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Mkuu wa shule ya sekondari Jumuishi ya Patandi Janeth Mollel anaishuruku serikali kupitia wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kwa kufanya uwekezaji huo ulioondoa changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye uhitaji maalum.

Anasema upande wa miundombinu shule hiyo imekidhi mahitaji yote ikiwemo njia za watoto wenye ulemavu wa viungo pamoja na vifaa vya ufundishaji na ujifunzaji.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameishukuru serikali kwa kuwaletea vifaa vinavyohitajika ili watimize ndoto zao za kielimu.

“Mimi ndoto yangu ni kuja kuwa mwanasheria ili nije kuwatetea wanyonge huko mtaani wanateseka, namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea vifaa vyote muhimu vya kujifunzia”- amesema mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo Muhiddin Igubuga.

Pia serikali imefanya ukarabati katika Chuo cha Ualimu PATANDI kinachofundisha walimu wa watoto wenye uhitaji maalum ili kuondoa changamoto chuoni hapo.

Mkuu wa Chuo hicho Lucian Segesela anasema ujenzi wa jengo jipya la utawala na uzio, ukarabati wa madarasa, mabweni, maabara na ununuzi wa vifaa vya kujifunzia umeongeza ari ya utoaji elimu bora na ufaulu.

“maboresho haya yamechangia udahili kwa mwaka umeongezeka kutoka wanachuo mia mbili hadi mia nne pia wanafunzi wenye ulemavu wana mazingira rafiki ya kujifunzia” amesema mwalimu Mkuu wa Chuo cha Patandi Lucian Segesela.

Katika kuhakikisha wanafunzi wa chuo hicho wanapata mafunzo bora ya vitendo, serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 158 kununua vifaa vya kujifunzia chuoni hapo.