Serikali yaweka wazi hatua inazochukua mwanamke akijifungulia gerezani

0
545

Serikali imesema kuwa endapo mwanamke atajifungua akiwa gerezani, kwa mujibu wa sheria atapewa muda wa kupumzika zaidi kuliko wafungwa wengine kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu, atatengwa, atapewa muda wa kuhudhuria kliniki, na atapewa chakula cha ziada na maziwa ili kufanikisha malezi ya mtoto aliyezaliwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Wananchi (CUF), Alfredina Apolinary Kahigi ambaye alihoji serikali haioni umuhimu wa kuwapumzisha bila kufanya kazi yoyote wanawake wanaojifungua wakiwa gereza kwa kipindi kisichopungua miezi sita ili wapate nguvu kwanza?

Masauni amesema kuwa huduma za wafungwa hao zimeainishwa vizuri katika Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Jeshi la Magereza kifungu namba 728 mapaka namba 729, toleo namba nne la mwaka 2003.

Aidha, Masauni amesema kwamba haiwezekani mwanamke akapata ujauzito akiwa ndani ya gereza, ni baada ya mbunge huyo kuuliza swali la nyongeza akitaka kujua mwanamke atachukuliwa hatua gani endapo atapata ujauzito akiwa ndani ya gereza.

Katika swali la pili kuhusu hatma ya mtoto atakayezaliwa ikiwa mama yake amefungwa muda mrefu Masauni amesema kuwa mtoto anapomaliza kunyonya maafisa wa ustawi wa jamii huenda magerezani na kuzungumza na wamama hao ili watoto hao waweze kulelewa na ndugu wengine, au taasisi nje ya gereza.

Hata hivyo ameongeza kuwa kwa kipindi chote ambacho mtoto anakuwa yupo na mama yake gerezani hupatiwa malezi bora ikiwa ni pamoja kupatiwa elimu ya awali katika shule ambazo zipo jirani na magereza.