Serikali yaweka makakati kuondoa umasikini kupitia kilimo

0
147

Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema ili kuondoa umaskini kwa jamii hapa nchini, Serikali imeweka mkakati wa kuona ni jinsi gani inaboresha maisha ya wananchi kupitia Sekta ya kilimo ambayo inachukua asilimia 70 ya Watanzania wote.

Kauli hiyo imetolewa na Kigahe wakati wa semina ya utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani iliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa bungeni mkoani Dodoma ikiongozwa
na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira David Kihenzile.

Aidha, semina hiyo imeandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo imewajumuisha wabunge wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Kamati ya kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa kuwepo kwa mfumo huo una tija kwani wakulima wanapata bei shindani ya mazao ya biashara na chakula kutokana na eneo husika na itasaidia kuwa na soko huria.

Naye Mrajisi Mkuu wa Tume ya Vyama vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege akitoa ufafanuzi juu ya maswali yaliyoulizwa na wabunge kuhusu sheria, amesema kuwa huo mfumo kama ukiimarishwa utakuwa mkombozi wa mkulima ambapo kama ushirika wako kwenye mchakato wa kukusanya maoni na kurekebisha sheria ya ushirika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wabunge wamesema kuwa mfumo huo utaenda kuwa mkombozi wa makulima huku wakiitaka Serikali kuhakikisha inaondoa changamoto zinazowakabili wananchi ili waweze kunufaika na mfumo huo .