Serikali yawataka wananchi kupunguza unywaji pombe

0
135

Serikali imewataka wananchi kupunguza ulaji wa vyakula vya mafuta, chumvi nyingi, unywaji pombe, kufanya mazoezi na kuacha kuvuta sigara ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari na shinikizo la damu.

Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuathiri jamii na yanachangia kwa takribani asilimia 40-45 ya idadi ya vifo vinavyotokea hospitalini, ikilinganishwa na asilimia 33 kwa miaka 5 iliyopita.

Wizara hiyo imehimiza kuwa tabia hizo zijengwe kuanzia ngazi ya familia na mashuleni ili kuwakinga watoto na kuwapa mwamko na kuchukua hatua hizo za kujikinga wakiwa katika umri mdogo.

Kuhusu magonjwa ya kuambukiza, hivi sasa UKIMWI umeendelea kuwa chini ya asilimia 4.7 huku idadi ya vifo vitokanavyo na UKIMWI vikipungua kwa asilimia 48 kutoka mwaka 2015, kifua kikuu maambukizi yamepungua kwa asilimia 23 na vifo kwa asilimia 33 kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Vivyo hivyo ugonjwa wa malaria vimepungua kwa zaidi ya asilimia 60 kati ya mwaka 2015 na 2020.