Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia shilingi bilioni 166.17 kwa ajili ya kugharamia mpango wa elimu bila malipo pamoja na kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapitio na Mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Pia amesema kuwa, Serikali imeboresha miundombinu ya shule za msingi 1,372, shule za sekondari 554 pamoja na shule 18 za Wanafunzi wenye mahitaji maalum. lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Kuhusu elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema Serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa kutoa mikopo kwa Wanafunzi 142,179.
“Shilingi bilioni 464 zitatumika kwa mwaka wa masomo wa 2020/2021 ikilinganishwa na shilingi bilioni 450 zilizotumika kwa wanafunzi 130,883 kwa mwaka 2019/2020,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema katika mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kuinua kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa kwa kuimarisha utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini, kutoa mafunzo kazini kwa walimu na wakufunzi pamoja na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Kuhusu suala la ukuzaji wa ajira na ujuzi, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, katika mwaka 2020/2021 Serikali imechukua hatua za makusudi hasa utekelezaji wa miradi ya kielelezo, ujenzi wa viwanda, pamoja na kuimarisha sekta binafsi kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania.
“Hadi kufikia Februari, 2021 ajira 594,998 zimezalishwa katika sekta mbalimbali, kati ya hizo, ajira 314,057 zimetokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ajira za Serikali, vilevile, ajira 280,941 zimezalishwa kupitia sekta binafsi,” amefafanua Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa masuala ya ukuzaji ajira na kazi za staha katika sera, mikakati na mipango mbalimbali ya kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata ujuzi stahiki pamoja na kuongeza fursa za ajira.