Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali haizuii ndugu wa marehemu kuchukua miili ya wapendwa wao kutokana na gharama za kuhifadhi miili hiyo, bali inafanya hivyo ili ndugu wa marehemu wamalizie madeni ya matibabu wakati akiwa mgonjwa.
https://www.youtube.com/watch?v=TjvW_bQ820I
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Faida Bakari aliyetaka kujua ni kwanini hospitali za umma zimekuwa zikizuia maiti kwa madai ya kulipwa madeni ya matibabu ya Marehemu, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa, serikali imeweka utaratibu wa msamaha kwa watu wasio na uwezo wa kulipia madeni hayo na kuruhusiwa kuchukua miili ya ndugu zao.
Ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa, vitengo vya Ustawi wa Jamii katika hospitali za serikali vimekuwa vikisikiliza na kutoa msamaha kwa Wananchi wasio na uwezo wa kugharamia matibabu ya ndugu zao na pia kuwapa msamaha na kuchukua maiti za ndugu zao na kwenda kuzihifadhi.
Aidha Waziri Ummy Mwalimu ametoa wito kwa Watanzania wote kujiunga na mifuko ya Bima za Afya ili kuepuka gharama kubwa za matibabu na pia kupunguza usumbufu wa kuzuiliwa kwa miili ya wapendwa wao kutokana na madeni ya matibabu.