Serikali yatoa msimamo watoto njiti kutibiwa bure

0
131

Serikali imesisitiza sera ya matibabu bure kwa Watoto wote na hata wale wanaozaliwa kabla ya muda wake (Njiti) mpaka watakapofikisha umri wa miaka mitano.

Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa ni sera ya serikali kuwa Watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano hata wale wanaozaliwa kabla ya muda wao (Njiti) kupatiwa matibabu bila malipo yoyote.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Agnes Hokororo, Dkt. Mollel amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusimamia utekelezaji wa sera hiyo kwenye maeneo yao ili Watoto wote wapatiwe matibabu bure.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave aliyetaka kujua mkakati wa serikali kupeleka kwenye hospitali na vituo vya afya vitu muhimu vya kujifungulia kwa kina mama ili wasilazimike kuvinunua wakienda kujifungua, Dkt. Mollel amesema, serikali imeweka sera ya kutoa huduma hizo bure lakini kuna maeneo vinakua havitoshi kutokana na wingi wa akina mama wanaojifungua katika maeneo hayo.

Dkt. Mollel amesema serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) wameanza mchakato wa kupeleka vifaa vya kujifungulia kwa kina mama kulingana na wingi wa mahitaji na sio aina ya kituo cha kutolea huduma.