Serikali yatenga hospitali maalumu kutibu corona

0
272

Serikali imetenga hospitali maalumu katika maeneo mbalimbali nchini, ambazo zitatumika kwa ajili ya kuwatibu wagonjwa wa homa ya corona watakaobainika nchini.

Akitoa taarifa ya serikali kwa wananchi kuhusu virusi vya corona, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa kwa mkoa wa Dar es salaam , hospitali hiyo maalumu itakua kwenye hospitali ya Mloganzila, mkoani Mwanza itakua Buswelu, Kilimanjaro itakua katika hospitali ya mawenzi, Zanzibar itakua katika hospitali ya Mnazi mmoja na Pemba itakua katika hospitali ya chake chake.

Hata hivyo amesisitiza kuwa kwenye maeneo ambayo tayari kuna hospitali, hospitali hizo maalumu kwa ajili ya kutibu corona zimetengwa katika maeneo ya pembeni.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, tayari serikali imepeleka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto shilingi milioni mia tano kati ya shilingi bilioni moja, fedha ambazo Rais John Magufuli ameagiza ziende huko baada ya kuahirisha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu.

Hapo jana, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitangaza kuingia nchini kwa virusi vya corona, ambapo mwanamke mmoja aliyeingia nchini machi 15 mwaka huu kutoka nchini Ubelgiji amegundulika kuambukizwa virusi hivyo.