Serikali yasisitiza watoto na wazee kulindwa

0
221

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kufanya tathimini juu ya fursa na changamoto zilizopo katika familia zao hususani kipindi hiki ambacho jamii inakabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akizungumza kuhusu siku ya Familia Duniani ambayo huadhimishwa Mei 15 ya kila mwaka.

Waziri Ummy amesisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanatumia kipindi cha mapambano dhidi ya corona kuwa karibu na familia zao, huku wakifanya ufuatiliaji wa karibu kwa watoto na Wazee hasa kuhusu hali zao za lishe na endapo kuna mabadiliko wawapeleke katika vituo vya kutolea huduma.

“Niwaombe wazazi na walezi muwe karibu na familia zenu hasa watoto na wazee na punde mnapobaini dalili za ugonjwa wa corona toeni taarifa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa”, amesisitiza waziri Ummy Mwalimu.

Amesema wakati dunia inaadhimisha siku ya familia na huku shule zikiendelea kufungwa, wazazi na walezi pia wana wajibu wa kubuni michezo mbalimbali pamoja na kuandaa mazingira bora yatakayowawezesha watoto kuendelea kufuatilia masomo kupitia vyombo vya habari na njia ya mtandao.

Kauli mbiu ya siku ya familia duniani kwa mwaka huu ni Familia ni Msingi katika kutokomeza corona, tuilinde na tuwalinde wengine.