Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, -Frank Chonya ahakikishe anawahamasisha Wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupata matibabu.
Ametoa agizo hilo mkoani Lindi alipokuwa akizungumza na Watumishi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa, alipotembelea hospitali hiyo akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Ruangwa.
Amesema kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kuwa na huduma ya Bima ya Afya ya Taifa, hivyo ni muhimu kwa Wananchi wengi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ambao unawawezesha kupata bure huduma za afya kwa kipindi cha mwaka mzima.
“Mkurugenzi hakikisheni fedha zote zinazokusanywa kupitia mfuko huu wa CHF zinaratibiwa vizuri na zinatumika kama ilivyokusudiwa, Mfuko wa Afya ya Jamii ni mkombozi katika utoaji wa huduma za afya kwa Wananchi, ni lazima wahamasishwe kujiunga nao,”ameagiza Waziri Mkuu.
Pia amemuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Dkt Salvio Wikesi kusimamia vizuri utoaji wa huduma kwa wagonjwa, kwa sababu baadhi ya Watumishi wanalalamikiwa kwa kutoa lugha zisizofaa kwa Wananchi wanaokwenda kutibiwa hospitalini hapo.
“Watumishi hapa mnalalamikiwa lugha mnazozitoa kwa Wagonjwa si nzuri, kila mmoja ajitafakari kuhusu utoaji wake wa huduma kwa Wagonjwa, badilikeni na muwe na lugha zinazowapa moyo Wagonjwa. Taaluma ya utoaji huduma za afya inahitaji kujitoa,”amesema Waziri Mkuu.
Baada ya kumaliza kikao chake na Watumishi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Ruangwa, Waziri Mkuu Majaliwa amehutubia Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Nachingwea, ambapo amewahakikishia kwamba ataendelea kushirikiana nao kuboresha maendeleo ya wilaya ya Ruangwa.