Serikali yasisitiza umakini katika utoaji vitambulisho vya Taifa

0
181

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Serikali imeagiza uwepo wa umakini katika utoaji wa vitambulisho vya Taifa hasa kwenye maeneo ya mpakani si kwa lengo la kumkomoa mtu, bali ni kwa ajili ya kuimarisha usalama wa nchi.
 
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Kagera, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Wabunge wa mkoa huo kuhusu usumbufu wanaoupata baadhi ya Wananchi wanapofuatilia vitambulisho vya Taifa kwani wengine wanadaiwa kuwa si raia.
 
Malalamiko hayo yametolewa wakati Waziri Mkuu akizungumza katika mkutano wa halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kagera ambapo yeye ni mlezi wa chama hicho mkoani humo.
 
“Watu tufuate taratibu katika suala ugawaji wa vitambulisho, Idara ya Uhamiaji wafuatilie kwa umakini kwa sababu lazima usalama wa nchi usimamiwe ipasavyo hususani katika mikoa ya mipakani, Watanzania mnatakiwa muwe makini msiruhusu watu kuingia kwa njia za panya kwani watu hao hawana nia njema,” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
 
Amesema lazima zoezi hilo lifanyike vizuri, na kwamba Serikali itaharakisha ili Wananchi waweze kupata vitambulisho.

Tayari Serikali imeongeza vifaa na Watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.