Serikali yasisitiza katazo la mifuko ya plastiki

0
134

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amelitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuongeza nguvu katika kusimamia utekelezaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo mara baada ya kuongoza zoezi la kufanya usafi katika soko kuu la wamachinga mjini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani hii leo.

Amesema ni lazima kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wanaokiuka agizo hilo pamoja na kuwataka watendaji wote wanaohusika kusimamia kwa karibu uzalishaji na matumizi ya mifuko mbadala.

Makamu wa Rais ameongeza kuwa ni vema kuhakikisha mifuko yote inayozalishwa inaonesha taarifa za mzalishaji na kama inakidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika.

Pia amesisitiza kampuni na watu binafsi wanaozalisha bidhaa za plastiki kuhakikisha taka zinazotokana na bidhaa zinazozalishwa zinakusanywa na kuondolewa.

Halikadhalika Makamu wa Rais amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kampuni zinazopewa kazi ya kuzoa taka zina uwezo kufanya kazi hizo kwa ufanisi.