Serikali yasema maandalizi ya uchaguzi mkuu yanaendelea vizuri

0
261

Idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzii wa mwaka huu  imeongezeka,  ambapo wapiga kura halali ni 29,804,992 ikilinganishwa na wapiga kura 23,161,440 wa mwaka 2015.

Akihitimisha mkutano wa 19 wa bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  inaendelea na uchambuzi wa taarifa za wapiga kura waliojiandikisha na baada ya zoezi hilo kukamilika, daftari la mwisho litakalotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu litaandaliwa na kuwekwa wazi.

Amewahakikishia Watanzania kuwa maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao yanayofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanaendelea vizuri na kwamba hakuna haja ya kuwa na wasiwasi na jambo hilo.

“Hivi sasa, pamoja na mambo mengine Tume imekamilisha matakwa ya sheria ya Taifa ya uchaguzi ya kufanya uboreshaji wa daftari la Kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu mmoja na mwingine,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini na wadau wengine wa uchaguzi kuzingatia katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.