Serikali yasema haijawanyima fursa ya masomo wanafunzi wanaopata mimba

0
265

Serikali imesema kuwa mkopo wa zaidi ya shilingi trilioni 1 uliotolewa hivi karibuni na Benki ya Dunia (WB) unaunga mkono jitihada za serikali za kuendelea kuinua elimu kwa shule za sekondari nchini.

Hayo yamesemwa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mkopo huo na suala la wanafunzi wanaopata ujauzito kutoruhusiwa kuendelea na masomo katika mfumo rasmi na kusisitiza kuwa msimamo huo umekuwepo miaka yote.

“Suala la wanafunzi wanaopata ujauzito kutoendelea na masomo halikuanza leo, ni msimamo wa serikali kwa miaka yote. Serikali iliweka mifumo ya elimu mbadala kwa wanafunzi wanaopata ujauzito. Mtoto wa kike aliyepata ujauzito hajanyimwa haki ya kusoma, ataendelea na masomo kwa utaratibu mwingine tofauti na ule rasmi ikiwemo vyuo vya maendeleo ya jamii na [vyo vya ufundi] VETA,” amesema Dkt Abbasi.

Aidha, amesema dhana ya kuzuia wanafunzi waliopata ujauzito kurudi katika mfumo rasmi wa elimu ni kutohamasisha wanafunzi kushiriki vitendo vya ngono wakiwa katika umri mdogo

Akizungumzia mkopo huo amesema kwamba utawanufaisha wanafunzi zaidi ya milioni 6 kwa mwaka, kwa kuhakikisha wanasoma katika mazingira bora, na pia sehemu ya mkopo itaimarisha mifumo na mazingira ya kumfanya mtoto asipate ujauzito ikiwemo kujenga shule na mabweni.