Serikali yasema ahadi yake kwa Kigoma iko palepale

Kigoma Tanzania

0
163

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewahakikishia Wakazi wa mkoa wa Kigoma kuwa, Serikali itaendeleza miradi yote iliyoanzishwa na uongozi wa awamu ya tano katika mkoa huo.

Dkt. Mpango ametoa.kauli hiyo wilayani Uvinza mkoani Kigoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani humo na kuongeza kuwa, ahadi ya Serikali ya kuunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa mingine kwa miundombinu imara ikiwemo barabara za lami iko palepale.

Akiwa katika wilaya hiyo ya Uvinza, Makamu wa Rais ameweka jiwe la Msingi la ujenzi wa mradi wa njia kuu ya kusambaza umeme wa kilovoti 132, unaotoka Tabora kuelekea mkoa wa Kigoma.

Ameitaka wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wizara ya Nishati kulipa fidia kwa wakati kwa Wananchi wote wanaostahili, ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Pia ameiagiza wizara ya Nishati kukamilisha mradi huo mwaka 2022, tofauti na ilivyopangwa awali kukamilika mwaka 2023.

Kazi nyingine aliyoifanya Makamu wa Rais Dkt.Mpango akiwa mkoani Kigoma ni kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kupoza umeme kinachojengwa katika eneo la Nguruka wilayani Uvinza.