Serikali yapokea msaada kutoka China kukabiliana na corona

0
288

Serikali imepokea msaada wa vifaa-tiba kutoka China kwa ajili ya kusaidia kukabiliana na mlipuko wa maambukizi ya homa ya mapafu inayoambukizwa na kirusi cha Corona (COVID-19), huku ikiishukuru kwa kushiriki kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammed Kambi amesema msaada huo ambao umetolewa na mfanyabiashara Jack Ma na taasisi yake ya Alibaba ni pamoja na mavazi (PPE) 1,000 ya kujikinga wakati wa kuhudumia watu waliobainika kuwa na homa hiyo, vitendanishi (Rapid Tests) 20,000 na barakoa (Masks) 100,000.

Prof. Muhammed amesema msaada huo utawasaidia wataalamu wa afya nchini wakati wa kuwahudumia waliobainika na watakaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

“Tumekuja hapa kushuhudia sehemu ya shehena ya tani tatu ya vifaa-tiba vilivyotolewa na Taasisi ya Jack Ma na Alibaba ambavyo vimewasili na ndege ya mizigo ya Jamhuri ya Shirikisho la Kidemokrasia Ethiopia,” amesema Prof. Muhammed.

Katika hatua nyingine, Prof. Muhammed amemshukuru afisa Ubalozi wa Ethiopia, Tewodros Girma ambaye amekabidhi msaada huo kwa niaba ya balozi wa nchi hiyo, Yonas Yosef.