Serikali yapiga marufuku ujenzi wa viwanda katika makazi ya watu

0
343

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, amepiga marufuku utoaji vibali vya ujenzi wa viwanda katika maeneo ya makazi ya watu katika wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Dkt Mabula ametangaza hatua hiyo wilayani Mkuranga, alipokutana na uongozi pamoja na Watumishi wa sekta ya ardhi wa wilaya hiyo, wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo, ziara iliyokua na lengo la kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kutatua migogoro ya ardhi.

“Mkuranga lazima uwe na mpango wa matumizi ya ardhi unaoonesha viwanda vikae wapi, siyo viwanda kujengwa kila kona, hiyo haipendezi”, amesema Naibu Waziri Mabula.

Kuhusu zoezi la Urasimishaji, Naibu Waziri huyo wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi ameuagiza uongozi wa wilaya ya Mkuranga kuliharakisha, ili kuepuka makazi holela na kuongeza kuwa ucheleweshaji wowote utasababisha
mji kutopangika.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, – Abdallah Ulega amesema kuwa, wilaya ya Mkuranga ina viwanda vingi kutokana kuwa na eneo linalovutia na kwamba atafurahi kama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itafanya jitihada za kuharakisha zoezi la urasimishaji.

‘’Kama serikali itaongeza kasi kidogo ya kupanga na kurasimisha maeneo ya wilaya hii basi itakusanya kiasi kikubwa cha fedha, maana Mkuranga imekuwa lango na ni kimbilio la Wananchi kutoka Dar es Salaam’’, amesema Naibu Waziri Ulega.