Serikali yapendekeza kuanzishwa Tuzo ya Aridhio kumuenzi Marin Hassan Marin

0
73

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, amependekeza kuanzishwa tuzo mbili katika kumuenzi marehemu Marin Hassan Marin, mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) aliyetutoka hapo jana, Aprili Mosi 2020.

Dkt. Hassan Abbasi ataja tuzo hizo kuwa ni ‘Tuzo ya Aridhio’ kwa ajili ya kuwaenzi wanahabari wanaofanya kazi nyuma ya kamera (behind the scene). ” Nyuma ya pazia, kuna watu wa kamera, kuna watu wa aina ya Marin ambao wanaongoza tukio zima.”

Mbali na tuzo hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali ameishauri TBC kuangalia suala zima la kuanzisha Tuzo/ Fellowship ya Marin Hassan itakayochukua vijana wanaotaka kuwa kama Marin ili “siku moja tuwe na kina Marin wengi.”

Katika mazungumzo kati ya yake na mtangazaji Asheri Thomas wa TBC, Dkt. Abbasi ameelezea namna Marin Hassan Marin alivyokuwa ni kioo cha wengi.

“Sisi ambao tuliingia baadae kwenye tasnia ya habari yeye ndio alikuwa mfano. Ni miongoni mwa watu wakati ule unamsikia kwenye redio hata kabla ya TV, ulikuwa unatamani kuwa mwanahabari,” amesema.

Marehemu Marin Hassan Marin, amefanya kazi TBC kwa kipindi cha miaka 15 hadi alipopatwa na umauti, ambapo amefanya vipindi mbalimbali vilivyompatia umaarufu kutokana na umahiri wake ikiwemo kipindi cha ‘Safari ya Dodoma,’ ‘Jambo Tanzania,’ na vilevile kuwa mmoja kati ya watu waliofanikisha kwa kiasi kikubwa TBC Aridhio, mfumo mpya wa upashaji habari wa TBC ulioanza rasmi Machi 30, mwaka huu.

Marin Hassan Marin amezikwa leo kisiwani Unguja katika eneo la Mwanakwerekwe.