Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi ametoa onyo kwa vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaozusha taarifa za maradhi, vifo bila kuzingatia misingi ya kisheria ya utoaji wa taarifa.
Dkt. Abbasi amesema kuwa kwenye kutoa taarifa zinazohusu umma wa Watanzania mfano magonjwa ya mlipuko zipo taratibu kwenye sheria za huduma ya jamii zinazoeleza ni kiongozi wa ngazi gani anapaswa kutoa taarifa kwa umma.
“Mtakumbuka mwaka jana Tanzania ilipopata janga la corona mheshimiwa Rais [Dkt. Magufuli] alitoa itifaki ya viongozi ambao watasemea maradhi haya ambapo ukiondoa viongozi wakuu wa kitaifa…,viongozi wengine waliopewa jukumu hilo ni Waziri wa Afya na mimi Msemaji Mkuu wa Serikali,” amesema.
Dkt. Abbasi ambaye pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari amesema utoaji wa takwimu na masuala mengine ya kisera kwenye maeneo haya yanapaswa kubaki kwa wasemaji rasmi na wataalamu ambao wana dhamana ya kufanya hivyo.
Amesema mpaka sasa nchi inakwenda vizuri na amewasihi viongozi wa dini kushiriki kutoa elimu wa wananchi wakiwahimiza kufuata miongozo ya wataalamu ili wasiwe na hofu.