Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Bharti Airtel leo zimetiliana saini makubaliano na uongezwaji wa umiliki wa hisa za serikali kutoka asilimia 40 hadi 49 na Airtel kubakia na hisa 51 kutoka hisa 60 za awali.
Akizungumza baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo Ikulu jijini Dar Es Salaam, Rais Dkt. John Magufuli amesema ongezeko hilo la hisa ni tija kubwa kwa taifa na kufanya uwekezaji wenye faida.
Amesema tangu kuanza kwa kampuni hiyo miaka tisa iliyopita hapa nchini Tanzania haijawahi kufaidika na gawio lolote na kwamba sasa makubaliano yamefikiwa.
Pia mbali na makubaliano ya uongezwaji wa hisa pia Tanzania itapatiwa shilingi Bilioni moja kila mwezi kwa muda wa miaka mitano kama fidia kutokana na serikali kutopata gawio lolote.
“Hii ni hatua nzuri kwa nchi kwani italenga kuleta wawekezaji wenye nia njema ya kuleta maendeleo kwa nchi ‘alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema makubalino hayo kufikiwa haikuwa rahisi ambapo ameipongeza kamati ya upande wa serikali iliyokuwa ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi aliyeongoza majadiliano na wawakilishi wa Kampuni ya Bharti Airtel mpaka kufikiwa kwa makubaliano hayo.
Katika makubaliano hayo suala la uongozi serikali itapendekeza Mkurugenzi Mkuu upande wa ufundi ambaye ataajiriwa na Kampuni ya Bharti Airtel kama makubaliano yanavyotaka kuwa katika uongozi wa kampuni hiyo kwamba serikali ya Tanzania itakuwa na kiongozi katika upande wa ufundi na Bharti Airtel wao watabaki na nafasi ya Mtendaji Mkuu na Mtendaji kwenye masuala ya fedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Bharti Airtel, Sunil Mittal ameshukuru kwa kampuni yake kufikia makubaliano hayo na serikali ya Tanzania kwani watahakikisha wanaendeleza uhusiano mzuri kwa makubaliano waliyofikia.
Mwenyekiti huyo ametoa kiasi cha shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii ambapo Rais Magufuli ametoa agizo kuwa fedha hizo zitakwenda kuongezwa katika Hospitali inayojengwa jijini Dodoma.