Serikali yaokoa shilingi trilioni 3.2 kwa mwaka

0
2071

Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi Trilioni 3.2 zikiwemo shilingi Trilioni 2.2 zilizookolewa kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kufanya uhakiki wa madeni ya serikali, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti feki.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James amesema timu ya wataalam wanaotengeneza na kusimamia mifumo ya mapato ya serikali, wakaguzi na wataalamu wa bajeti pia imefanikiwa kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za serikali baada ya kuunganisha taasisi 304 katika mfumo unaodhibitiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Katibu Mkuu huyo amebainisha hayo wakati akiwasilisha taarifa ya uanzishwaji wa mifumo katika taasisi za umma 304 kwa Rais Dkt. John Magufuli Ikulu jijini Dar Es Salaam na kusema fedha hizo zimeokolewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2017/18.

Aidha Rais Dkt. John Magufuli amewapongeza wataalamu hao kwa kazi nzuri waliyoifanya na kumuagiza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kuhakikisha taasisi zote za serikali zinazopaswa kuunganishwa na mifumo ya udhibiti zinaunganishwa haraka iwezekanavyo.

Amesema fedha zilizopatikana baada ya udhibiti wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato zimesaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya 208, ujenzi wa hospitali mpya 67, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa Standard Gauge Railway, madaraja, barabara, kusambaza umeme na maji.