Serikali yalia na mradi wa Mkulazi

0
220

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama, ameiagiza kamati elekezi ya kusimamia mradi wa Mkulazi Estate uliopo mkoani Morogoro kuhakikisha ujenzi wa barabara pamoja na uwekaji umeme  unafanyika ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Waziri Mhagama amesema ujenzi wa barabara pamoja uwekaji umeme kwenye eneo la mradi, kutawezesha kuzalishwa kwa tani laki mbili za sukari kwa mwaka.

Ameitaka kamati hiyo kuwasilisha haraka iwezekanavyo mpango wa namna itakavyotatua changamoto hizo ndani ya kipindi cha wiki mbili.

“Maamuzi yalifanyika Novemba na hadi leo Machi hakuna kilichofanyika kwenye kufuatilia, nataka mwezi huu wa tatu kabla haujaisha mitambo ianze ujenzi wa barabara hapa na nataka majibu ya lini shughuli za kuweka umeme hapa zinaanza, huu ni mradi wa kimkakati kwani tunao upungufu wa tani 200,000 za sukari ambazo zitazalishwa hapa,”amesema Waziri Mhagama.

Kampuni hodhi ya Mkulanzi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuzalisha tani laki mbili na nusu za sukari kwa mwaka, ili kupunguza nakisi ya mahitaji ya sukari nchini.

Endapo mradi wa Mkulazi Estate ukianza kutekelezwa, unatarajia kuzalisha tani laki mbili za sukari kwa mwaka.