Serikali yakemea upotoshaji Loliondo na Ngorongoro

0
89

Serikali imesisitiza kuwa kinachoendelea katika eneo la Loliondo mkoani Arusha ni uwekaji wa alama za mipaka kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya hifadhi hapa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Maurus Msuha amesema, lengo ni kutenganisha maeneo ambako shughuli za kibinadamu zinaendelea na kule ambako haziruhusiwi na kwamba hakuna mtu anahamishwa kutoka kwenye eneo hilo.

Dkt. Msuha amesema, katika wilaya ya Ngorongoro serikali inaendesha mazoezi mawili kwenye maeneo mawili tofauti na kila zoezi limepangwa kulingana na mahitaji ya eneo husika na hakuna muingiliano wowote.

Amesema kuwa katika eneo la pori tengefu la Loliondo, serikali inaweka mipaka kutenganisha eneo la kilomita za mraba 2,500 kwa ajili ya wananchi na kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi wa eneo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa mfumo wa ikolojia ya hifadhi ya Serengeti.

Dkt. Msuha ameeleza kuwa serikali itaweka mpango bora wa matumizi ya ardhi ya eneo la Loliondo, ili kusitokee muingiliano baina ya maeneo ya wananchi na eneo la hifadhi.