Serikali imewahakikishia wakulima wa pamba nchini kuwa itaendelea kufuatilia upatikanaji wa viuadudu vya zao hilo na kuhakikisha vinawafikia wakulima kwa wakati.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameyasema hayo leo bungeni wakati akijibu swali la swali la Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku Musukuma aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani kupeleka dawa za kuuwa wadudu wa pamba kwani zinazopatikana huwa ni chache.
Bashe amesema katika msimu wa mwaka 2019/2020 eneo la ekari 1,786,890 za pamba limelimwa na kuzalisha kiasi cha tani 350,473 ambapo chupa milioni 8.2 zenye thamani ya Tsh bilioni 41 na vinyunyizi 20,000 vyenye thamani ya shillingi bilioni 1.6 vilinunuliwa.
Amesisitiza kuwa si sahihi kusema kuwa serikali inahamasisha kilimo cha pamba ikiwa haina uwezo wa kupeleka sumu za kuulia wadudu, na hata zinapopatikana huwa ni chache. Amesema serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao likiwemo zao la pamba ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Akizungumzia uchache wa viuadudu vya zao la pamba Bashe amesema kuwa umechangiwa na baadhi ya wakulima kutumia viuadudu katika kupulizia mazao mengine kama vile mahindi na viazi vitamu ili kudhibiti viuavijeshi vamizi.
Vilevile, amesema kuwa kukosekana kwa uaminifu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji katika baadhi ya maeneo ukiwemo Mkoa wa Geita ambapo viuadudu vilivyopelekwa viliuzwa katika maduka ya pembejeo kinyume na taratibu za usambazaji wa viuadudu vya zao la pamba.
Kutokana na vitendo hivyo watu zaidi ya 12 walikamatwa na kati yao watu tisa walifunguliwa mashtaka, ambapo watu nane walihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja.