Serikali yaja na mkakati kukuza utalii wa ndani

0
121

Katika kukuza sekta ya utalii nchini na  kuongeza mwamko wa Watanzania kutembelea vivutio vya utalii,  Wizara ya Maliaasili na utalii inafanya utafiti ambao utaangazia utalii wa ndani na  mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika uzinduzi wa utafiti wa utalii wa ndani na mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa nchi yetu kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO19, Waziri wa Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amesema ni mara ya kwanza kufanyika utafiti wa aina hii tangu uhuru.

Amesema sekta ya utalii ina mchango mkubwa nchini ambapo inatoa ajira milioni 6, asilimia 25 ya fedha za kigeni na 60% ya mauzo ya huduma.

Ameongeza kuwa utafiti huo ambao unatarajiwa kufanyika kwa miezi minne ikiwa ni sehemu ya matumizi ya mkopo wa shilingi trilioni 1.3 za Benki ya Dunia, utawezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maaendeleo na Ilani ya CCM ambayo inataka watalii wafike milioni 5 na mapato $6 bilioni ifikapo mwaka 2025.

Awali akitoa muhtasari kuhusu utafiti huo, Dkt. Ladislaus Batinolohu kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambaye ni mshauri elekezi wa utafiti huo amesema lengo kubwa ni kujua mchango wa utalii wa ndani katika uchumi wa nchi, na hatua za kuchukuliwa kuboresha.

Kuhusu utekelezaji  wake amesema utafanyika katika wilaya zote nchini, na katika kila wilaya watatembelea kata mbili,  na kila kata watatembelea vijiji viwili, ambapo kwa ujumla watatembelea kaya 33,800.

Kwa mwaka 2020/21 Tanzania ilipata watalii zaidi ya milioni 1.6, ambapo kati yao 700,000 walikuwa watalii wa ndani.