Serikali yaja na mkakati kuinua zao la Mkonge

0
167

Serikali imedhamiria kuinua kilimo cha mkonge katika mikoa inayolima zao hilo ili liweze kukuza kipato cha mwananchi na nchi kwa ujumla.

Akizungumza na wananchi mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya shamba la mkonge lililopo Kigombe mkoani Tanga Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, mkonge ni zao la kibiashara na halihitaji mtaji mkubwa kuanzisha hivyo hata mwananchi wa kawaida anaweza kulima.

“Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha zao hili linalimwa na wananchi wa kawaida, kilimo cha mkonge ni rahisi Hekari moja ambayo mtu wa kawaida anaweza kulima inaweza kumgharimu kiasi kidogo cha pesa, mche mmoja unauzwa shilingi mia mbili kwa hiyo kwenye hekari moja itahitaji shilingi laki tatu na ishirini kupata miche yote ya kupanda”-Amesema Waziri Majaliwa

Kuhusu masoko ya mkonge Waziri Mkuu amesema masoko yapo, kinachotakiwa ni kulimwa zao hilo kwa wingi kwani serikali inasimamia biashara hiyo na kudhibiti mianya yote ya udanganyifu.

“Tengeni maeneo yenu, eneo lingine limeni mazao yenu ya kila siku lingine limeni mkonge, huku unavuna mahindi na huku una uwekezaji wako wa mkonge. Mkonge ni fursa ya kibiashara, katika kuanza hili jana tumezungumza mambo mengi na tulipeana maelekezo na wakuu wa wilaya kwenye eneo hili tunaanza kwa kupatikana kwa mbegu”-Amesema Waziri Majaliwa

Waziri Mkuu yupo mkoani Tanga kwa ziara ya siku tatu yenye lengo la kupokea taarifa na kukagua uzalishaji wa zao la mkonge mkoani humo na mikoa jirani ikiwa ni mkakati wa kuinua zao hilo.