Rais John Magufuli amebatilisha pendekezo la kufutwa shamba lenye ukubwa wa Ekari Elfu Moja lililopo Kidunda wilayani Mvomero mkoani Morogoro, linalomilikiwa na Cecilia Rusimbi.
Uamuzi wa Rais Magufuli wa kubatilisha ufutaji wa shamba hilo unatokana na kubainika kuwa sababu zilizowasilishwa za kutaka kufutwa kwa shamba hilo ambazo ni kutoendelezwa, hazikuwa na ukweli na zililenga kumdhulumu mmiliki wake.
Akitangaza uamuzi huo wa Rais Magufuli wilayani Mvomero, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema kuwa, baada ya kufuatilia mashamba yaliyopendekezwa kufutwa, Rais amebaini taarifa alizopelekewa za kufuta shamba la Cecilia hazikuwa sahihi na hivyo kuamua kubatilisha pendekezo lililowasilishwa kwake na kumpatia haki yake mmiliki.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Lukuvi amewaonya Maafisa ardhi nchini kuhakikisha wakati wa kufanya zoezi la ukaguzi ama upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa wanazingatia haki pamoja na kufuata sheria, badala ya kufanya kazi hiyo kwa upendeleo ama kumuonea mtu.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi amesema kuwa utendaji kazi wa Maafisa Ardhi katika wilaya ya Mvomero umekuwa si wa kuridhisha na usiozingatia maadili, jambo linalosababisha wilaya hiyo kuongoza katika mkoa wa Morogoro kwa kuwa na migogoro mingi ya ardhi pamoja na malalamiko mengi ya Wananchi dhidi ya Maafisa hao.
“Baadhi ya watumishi katika ofisi ya halmashauri ya wilaya ya Mvomero mnajifanya ni Maafisa ardhi au Wapimaji wakati hamkuajiriwa kwa nafasi hiyo, mnasaini nyaraka za ardhi na kuwaumiza wananchi” amesema Waziri Lukuvi
Kwa upande wake Cecilia Rusimbi amemshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kubatilisha ufutaji shamba lake, na kuuelezea uamuzi huo kuwa umezingatia haki.
” Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987 na kuhangaikia hati kwa muda mrefu na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba langu liko katika mpango wa kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii imenifanya kuishi kwa wasiwasi”,amesema Cecilia.
Waziri Lukuvi ameagiza shamba hilo ambalo ni la kilimo cha Michikichi, Mitiki na Bamboo kupangwa upya na mmiliki wake kupatiwa hati kulingana na upimaji utakaofanywa na kumtaka kuliendeleza kwa mujibu wa sheria.