Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itachambua kwa kina na kutatua kero zote ambazo zimeanishwa katika ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Akizungumza mara baada ya kupokea ripoti ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali imeyapokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na NEC kwa lengo la kuboresha uchaguzi mkuu ujao.
Rais Samia ramesema serikali itaangalia namna ya kuwa na chombo cha kusimamia uchaguzi mkuu na ule wa serikali za mitaa kama ambavyo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji wa Mahakama Kuu, Semistocles Kaijage katika taarifa yake ya uchaguzi.
Aidha, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kuwa makini wakati wa kujaza fomu ili kuondoa kasoro zinazojitokeza na kutoa mwanya kwa chama tawala kupata viongozi wengi wanao pita bila kupingwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jaji Kaijage amesma uchaguzi uliopita ulikuwa na changamoto kadhaa ambazo hata hivyo hazikuathiri uchaguzi wenyewe.
Jaji Kaijage ameongeza kuwa Tume imepata mafanikio makubwa katika uchaguzi uliopita kwani wameweza kutangaza matokeo ya urais ndani ya saa 48 kama ambavyo sheria inawataka kufanya.
Kukabidhiwa kwa ripoti hiyo kumetoa nafasi kwa NEC kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
