Serikali yaagiza wakulima kugawiwa mbolea bure

0
490

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ihakikishe mbolea iliyotolewa bure kwa wakulima wadogo inawafikia na kuwanufaisha wahusika kama lengo la kampuni ya YARA lilivyokusudia.

“Nawasihi Wizara ya Kilimo msimamie ugawaji wa mbolea hii na nisingependa kusikia kuwa baadhi ya watu wasiowaaminifu wanajinufaisha kwa kuwauzia wakulima mbolea hii. Serikali ya Tanzania imejizatiti katika kukuza na kuboresha kilimo nchini kwa kuwa zaidi ya 80% ya Watanzania ni wakulima,” ameongeza Waziri Mkuu.

Majaliwa amesema idadi kubwa ya wakulima wanaokadiriwa kuwa 75% ni wale wenye uwezo wa kulima hekari moja hadi tano na sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo wa kumudu gharama hasa pembejeo na viuatilifu.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema lengo kuu ya programu ya ugawaji mbolea bure kwa wakulima ni kuongeza tija kwa uzalishaji wa mazao ya chakula hasa mahindi na mpunga.

Hasunga amesema mbolea hiyo imefanyiwa utafiti na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuthibitishwa kuwa inafaa kwa matumizi katika mazao ya mahindi na mpunga nchini na inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya YARA Tanzania, Winstone Odhiambo katika hotuba yake amesema mbolea itakayogawiwa ni aina NPK tani 12,500 yenye thamani ya shilingi bilioni 16.5.

Amesema utaratibu unaotumika kuwapata wanufaika wa mbolea hiyo ni kwa wakulima kujisajili kwa kupiga 14946*16# na amewaomba wakulima waendelee kujisajili kwa wingi.