Serikali yaagiza kiwanda cha Mponde kianze kazi

0
2293

Serikali imemaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya wakulima wa chai wa wilaya za Lushoto na Korogwe zilizopo mkoani Tanga  na kampuni ya Mponde Tea Estate uliosababisha kufungwa kwa kiwanda cha chai cha Mponde na kuagiza kiwanda hicho kianze kazi mara moja.

Uamuzi huo wa serikali umetangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kweminyasa kata ya Mponde wilayani Lushoto baada ya kutembelea kiwanda hicho.

“Waziri Mwijage na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Profesa  Siza Tumbo hakikisheni kazi ya kukagua kiwanda na mitambo inafanyika haraka na kubaini mitambo ipi ni mizima na ipi ina hitilafu ili ukarabati ufanyike na kiwanda kianze kazi mara moja,”ameagiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa mwaka 1999 serikali iliamua kuwapa wakulima wa chai kiwanda hicho  kwa ajili kuwawezesha kuwa na sehemu ya kuchakata chai yao, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi na hivyo imeamua kukirudisha serikalini baada ya kuwepo kwa migogoro iliyoathiri uzalishaji.

“Serikali imeamua kukichukua kiwanda hiki ambacho awali ilikikabidhi kwa wakulima wa chai na kwamba itahakikisha lengo lake la kuboresh kilimo linafanikiwa na  wakulima wanaendelea kulima zao la chai, hatutaki kusikia masuala ya Utega wala Mponde hapa si mahali pake,”amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa anayeendelea na ziara yake mkoani Tanga.

Kuhusu suala la madeni ya watumishi, ameagiza watafutwe na madai yaorodheshwe kwa ajili ya malipo, na amewahakikisha wananchi hao kuwa ajira zilizopotea baada ya kiwanda hicho kufungwa zitarudi kwa kuwa serikali inataka kuona kiwanda hicho cha chai cha Mponde kinafanya kazi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, wakulima hao wa chai wa wilaya za Lushoto na Korogwe walikosea kwa kuunda Umoja wa Wakulima wa Chai (UTEGA) ambapo katika kusajili badala ya kuanzisha ushirika wao walisajili kama NGO ambayo ilikuwa na wanachama wake, huku kiwanda kikiwa kimeanzishwa kwa ajili ya wakulima wote, jambo ambalo lilisababisha mgogoro baina ya wakulima na viongozi wa UTEGA.

Ameongeza kuwa wakati mgogoro huo ukiendelea kati ya UTEGA na wakulima wa chai wasiokuwa wanachama wa NGO hiyo, uliibuka mgogoro mwingine baina ya wakulima wote pamoja na mwekezaji ambaye ni kampuni ya Mponde Tea Estate baada ya kukabidhiwa kiwanda hicho  na uongozi wa UTEGA bila ya wao kushirikishwa.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makam wa Rais Muungano na Mazingira, –  January Makamba alisema kuwa mgogoro huo wa kiwanda cha Mponde ulianza mwaka 1999 na ilipofika mwezi Mei mwaka 2013, wananchi walimlalamikia kwa kushindwa kutatua tatizo hilo.

Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli pia  ameiomba serikali iwasaidie wakulima wa zao la chai  kwa kuwapa miche mipya pamoja na pembejeo kwa ajili ya kufufua zao hilo na kukiwezesha kiwanda cha chai cha MPonde kupata malighafi kama ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza  kiwandani hapo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji  Charles Mwijage amesema kuwa  tayari wataalam kwa ajili ya kukagua mashine zote zilizopo kiwandani hapo wamekwishafika kiwandani ili mchakato wa kuziwasha mashine hizo uanze  mara moja.