Serikali kusaidia kuanzishwa benki ya WAWATA

0
222

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kuwa serikali itasidia kuanzishwa kwa benki ya umoja.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akihutubia katika Jubilei ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo amesema wazo la WAWATA kuanzisha taasisi ya kifedha linaungwa mkono na Serikali na kuelekeza lishughuikiwe mara moja.

“Nimesikia WAWATA mnapanga kujenga uwezo na kuwaweka pamoja wanawake wa kikatoliki katika vikundi vya kuweka na kukopa ili wapate mtaji wa biashara ndogondogo za kiuchumi. Sasa mnawazo la kwenda mbali zaidi kuanzisha ‘microfinance’ ya WAWATA, hapa niseme Serikali itawapa msaada wote unaohitajika ili muweze kulitimiza hili,” amesisitiza Rais Samia.

Aidha, amepongeza juhudi za WAWATA kuhakikisha usalama wa watoto kwa kutoa elimu ya ulinzi kwa watoto. Huku akigusia kuwa mshikamano baina ya wanawake ni jambo la msingi.

“Changamoto ya mwanamke mmoja wa Tanzania, ni changamoto ya mwanamke yeyote yule,” ameongeza Rais Samia.

Amewapongeza pia WAWATA kwa kushiriki vyema kwenye utunzaji wa mazingira kwa kuotesha miti 530,416 mara dufu zaidi ya kiwango walichojiwekea cha kupanda miti 34, 000.

Mbali na mazuri hayo Rais Samia, amewataka WAWATA kuzidi kuongeza nguvu kwenye malezi bora ya watoto na vijana haswa wakati wa kipindi hiki cha mmomonyoko wa maadili.