Serikali kununua korosho kwa sh 3,300

0
1675

Rais John Magufuli ametangaza kuwa, serikali itanunua korosho za wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa shilingi elfu 3, 300 kwa kilo muda wowote kuanzia hivi sasa.
Rais Magufuli ametoa tangazo hilo Ikulu Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri wawili na Naibu Mawaziri wanne aliowateua hivi karibuni.

Akitoa tangazo hilo, Rais Magufuli amesema kuwa serikali imeachana na kampuni 13 ambazo zimejitokeza hadi asubuhi ya leo kuonyesha nia ya kununua korosho hizo baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Rais Magufuli amesema kuwa serikali imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa, kampuni hizo hazina nia njema na wakulima wa zao hilo la korosho la lengo lao ni kuendelea kuwanyonya.

Amewataka viongozi hao aliowaapisha hii leo ambao ni pamoja na wa wizara nyeti za Kilimo na Viwanda, Bishara na Uwekezaji kufanya jitihada za kutafuta soko la korosho kwa kuwa kwa sasa jitihada hazijafanyika ipasavyo.

Pia ametumia hafla hiyo kuiagiza wizara inayohusika na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kumthibitisha kwenye nafasi ya Ukurugenzi aliyekua akikaimu nafasi hiyo.

Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuwa hadi kufikia asubuhi ya leo, kampuni 13 zimejitokeza zikithibitisha kuwa zitanunua korosho kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali baada ya kuwapatia muda wa siku nne kuthibitisha jambo hilo.

Waziri Mkuu pia amewataka viongozi wote walioapishwa, kujifunza kwa haraka majukumu yao na kutekeleza majukumu hayo kwa uadilifu na nidhamu