Serikali kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua

0
208

Serikali imepanga kutumia fungu la dharura kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua, ikiwemo barabara za wilaya za Handeni, Korogwe, Lushoto na Pangani mkoani Tanga.

Akijibu swali Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa amesema kuwa, pamoja na kukarabati barabara hizo Serikali pia inaendelea na ujenzi wa miradi ya barabara ikiwemo ile ya kutoka Handeni – Mziha – Dumila hadi Gairo na ile ya kutoka Handeni hadi Singida.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, – Omar Mgumba ameliambia Bunge kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri yenye lengo la kuboresha zao la kahawa.

Amesema kuwa, mazingira hayo mazuri ni pamoja na kutoa mafunzo kwa Wakulima wa Kahawa kuhusu upanuzi wa mashamba, matumizi ya mbegu bora zinazostahimili ukame na magonjwa pamoja na matumizi ya mfumo wa minada katika uuzaji wa zao hilo.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Bunge limeendelea kwa kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2019.