Serikali kujenga shule elfu moja

0
146

Serikali imesema inatarajia kujenga shule za sekondari elfu moja ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa kwa wanafunzi wanaofaulu kujiunga na elimu ya sekondari nchini.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema hayo katika ziara ya kukagua miundombinu ya elimu kwa shule za sekondari wilayani Kongwa Mkoani Dodoma ambapo amesema serikali inaendelea kukarabati miundombinu ya shule ili kuongeza viwango vya ufaulu.

Profesa Ndalichako amesema ili kukabiliana na uhaba wa shule na vyumba vya madarasa hapa nchini Serikali imepanga kujenga shule za sekondari elfu moja.

Kwa upande wake Spika wa Bunge Job Ndugai anasema uchache wa miundombinu ya madarasa unaathiri kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi wilayani humo.

Spika Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa amesema, kumekuwa na matokeo yasiyo ya kuridhisha kwa wanafunzi wa kidato cha nne yanayochangiwa na uhaba wa vyumba vya madarasa kwenye shule za wilayani humo.