Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanza jitihada za kufuta tozo zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini, zikiwemo zile za kwenye pembejeo, ili kuwawezesha wafanyabiashara kuzifikisha hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya Papo kwa Papo kwa kwa Waziri Mkuu na kuongeza kuwa Serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wauzaji wa pembejeo juu ya tozo hizo.
“Serikali imesikia vilio vyenu na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni aina gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha ili muendelee kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema kuwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa wafanyabiashara na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini, ikiwemo ya pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba tayari Mawaziri wa kisekta wenye dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye wizara zao zinazokwamisha ufanyaji biashara katika mazingira rafiki wameshakutana, kwa ajili ya kujadili namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
