Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, Serikali inafanya marekebisho ya Sera za Taasisi zinazosimamia kazi za Sanaa na Ubunifu nchini, ili kuziwezesha Taasisi hizo kuwahudumia Wasanii kwa ufanisi.
Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa Tamasha la Sanaa la Mwalimu Nyerere, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa, mabadiliko ya Sera za Taasisi hizo yatawawezesha Wasanii kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia amewataka Wasanii nchini licha ya changamoto zinazowakabili kutumia kazi zao za Sanaa kuifahamisha jamii mambo mbalimbali ya maendeleo yanayofanywa na Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo.
Amesisitiza kuwa, Serikali inatambua mchango mkubwa ambao umekua ukitolewa na Wasanii na kwamba itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa ametamka kuwa Tamasha hilo la Sanaa la Mwalimu Nyerere linatakua likifanyika kila mwaka na ameshauri wakati wa Tamasha hilo kuwepo na maonesho ya kazi mbalimbali za Sanaa.
Wakati wa Tamasha hilo, umeanzishwa Mfuko wa Wasanii, na Viongozi mbalimbali waliohudhuria Tamasha hilo wameweza kuuchangia, huku Rais John Magufuli akichangia Shilingi Milioni Mia Moja na Waziri Mkuu Majaliwa amechangia Shilingi Milioni Tano.
Zaidi ya Shilingi Milioni 140 ambazo ni ahadi zimepatikana kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo wa Wasanii.
