Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt Hassan Abbasi ametoa taarifa inayohusu mafanikio ya kijamii na kiuchumi yaliyofikiwa na serikali katika kipindi cha miaka mitatu.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Dkt Abbasi amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli imeendeleza mageuzi ya kiuchumi yenye lengo la kuwaletea Watanzania maendeleo.
Amesema kuwa ndani ya kipindi hicho cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli, uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa kasi inayokubalika duniani, mbali na changamoto kadhaa zinazojitokeza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, mambo yanayosimamiwa na serikali ya awamu ya tano ni pamoja na ukusanyaji wa mapato, ufufuaji wa mashirika ya umma, mapambano dhidi ya rushwa na usimamiaji wa miradi ya maendeleo.