Serikali kuendelea kuwawezesha vijana

0
142

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana kwa mafunzo na mitaji, ili kuwapa uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Akijibu swali la Mbunge wa viti Maalum Ng’wasi Kamani, Waziri Mkuu amesema serikali ilitenga shilingi bilioni moja na kuongeza shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi na kisha kupewa mitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema licha ya ukweli kuwa fedha hizo hazitoshi lakini serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wanaendelea kutenga fedha kupitia mpango wa kuwawezesha vijana kwenye asilimia 10 za mapato ya kila halmashauri.

Ameongeza kuwa kwa sasa serikali inashirikiana pia na sekta binafsi katika kuwawezesha vijana kupata ujuzi na kujitegemea kupitia mafunzo yanayotolewa katika vyuo na taasisi mbalimbali za ufundi hapa nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa amewataka vijana kuwa na maeneo maalum ya kufanyia shughuli zao ili kuwawezesha kufikiwa na taasisi za fedha pamoja na serikali na kupatiwa ujuzi na mikopo kwa ajili ya kufanikisha shughuli hizo.